Ujue ugonjwa wa akili uitwao #Skizofrenia au #Schizophrenia

Skizofrenia ni ugonjwa wa akili ambao unaadhili jinsi ya kufikiri, utambuzi, tabia na hisia. Baadhi ya dalili za ugonjwa huu ni kama vile:

  1. Kuchanganyikiwa
  2. Kushindwa kufikiri sawasawa
  3. Mabadiliko makubwa ya kitabia yanayoathiri utendajikazi wa mtu
  4. Kuwa na imani isiyo ya kweli
  5. Kuongea visivyojulikana au kueleweka
  6. Kuona vitu ambavyo watu wengine hawaoni

Zaidi ya dalili za ugonjwa huu ni kwamba:

Mgonjwa husikia sauti ambazo watu wengine hawasikii. Sauti hizi zinaweza kuwa zinaongea zenyewe kwa zenyewe, au zinamuongelesha mgonjwa au zinamuahamurisha.

Kwa kawaida sauti hizi huwa zina nguvu sawa na sauti halisi kwa kiasi ambacho mgonjwa huziitikia na kufuata, au kuzitii.  Hili linaweza kupelekea mgonjwa kujidhuru au kuwadhuru watu wengine au kufanya matendo ambayo si ya kaiwada hata kama hayana madhara ( abnormal behaviours).

Mgonjwa pia hupata hali ya kuwa na imani kali sana yenye nguvu juu ya jambo fulani lakini jambo hilo ni la uongo au halipo. Mfano anaweza kuamini kuwa yeye ni Afisa Usalama wa Taifa, au Yeye ni mungu au ni kiongozi wa nchi na mfano wa hayo.

Pia ugonjwa huu humletea mabadiliko makubwa mgonjwa ya kitabia na kimuonekano.

Watu waishio na Skizofrenia huhitaji matibabu ya muda mrefu na hata kutumia dawa maisha yao yote.

Kupata matibabu mapema kunaweza kusaidia kupunguza ukali wa dalili na hivyo kumfanya mgonjwa kuweza kujitegemea na kuboresha maisha yake.

Jamii yetu kwa kukosa uelewa huwachukulia kama waliorogwa au kwamba hawawezi kutibiwa na kurejea hali zao za awali (japo watalazimika kutumia dawa muda mrefu au kwa maisha yao yote), hili limepelekea kuwatelekeza wagonjwa wa Skizofrenia wakiishi mitaani.

Kwa kuishi kwao mitaani hali ya ugonjwa inaongezeka, aghalabu hupata maradhi mengine na hata maambukizi kwa sababu ya kula, kulala na kuishi maisha yasio na afya.

Leave a comment

1 × two =